
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali itajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme eneo la Dumila, Kilosa, Mhe. Kapinga amesema Serikali kupitia TANESCO itatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Morogoro hadi Dumila yenye urefu wa kilomita 66 pamoja na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katika eneo la Magole – Dumila kupitia mpango wa Gridi Imara awamu ya pili unaotarajia kuanza mara tu baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza mwaka 2026.
Mh. Kapinga ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilosa. Mhe. Palamagamba Kabudi aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme eneo la Dumila, Kilosa.
Kuhusu Serikali kuimarisha Ofisi ya TANESCO Dumila ili iweze kutoa huduma bora Mhe. Kapinga amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma kwa wanachi ili waendelee kupata umeme wa uhakika.
Ameongeza kuwa, maelekezo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ni kuhakikisha wafanyakazi wa TANESCO wanafanya kazi kwa weledi na kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za umeme katika maeneo yote Tanzania.
Akijibu swali la Mbunge wa Mbinga Vijijini, Mhe. Benaya Kapinga kuhusu ni lini Serikali itajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme Wilaya ya Mbinga, Mhe. Kapinga amesema mradi wa kituo hicho upo katika hatua za utekelezaji na unatakiwa kuanza awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza kukamilika.
Ameongeza kuwa, Serikali itausimamia mradi huo kwa weledi na nguvu ili uweze kukamilika na kuongeza kuwa Serikali imeboresha njia ya umeme ambayo inapeleka umeme kutoka Songea hadi Mbinga na laini za Mbinga Vijijini.
Vilevile, kuhusu swali la Mhandisi Mhe. Samweli Ayuma, Mbunge wa Hanang ambaye alitaka kufahamu ni lini kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Hanang kitajengwa, Mhe. Kapinga amesema kipo katika awamu ya pili ya utekelezaji.
