Back to top

Vyuo na kidato cha sita kufunguliwa Juni Mosi.

21 May 2020
Share

Rais Dkt.John Pombe Magufuli amesema vyuo vyote nchini na kidato cha sita  vitafunguliwa  Juni mosi mwaka huu, baada ya serikali kujiridhisha na mwenendo wa kupungua kwa maambukizi ya virusi vya Corona.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma baada ya kuwaapisha baadhi ya viongozi aliowateua hivi karibuni.

Aidhaameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iandae utaratibu wa kuwawezesha kukamilisha muhula wao wa masomo na kufanya mitihani ya taifa bila kupoteza muda.

Kwa wanafunzi wengine wa shule za sekondari na msingi amesema serikali inajipa  muda kidogo kuangalia hali ya  kupungua kwa maambukizi ya virusi hivyo.

Kuhusu michezo Rais ameruhusu iendelee kuanzia Juni Mosi 2020.

Aidha amesema Mei 27 na 28 ndege za watalii zitaanza kuingia nchini na kufafanua kuwa hawatalazimika kuwekwa  karantini kwa siku 14, bali watapimwa kujua hali zao na kama wako vizuri wataendelea na safari ya utalii.

Kuhusu misaada inayotolewa ya vifaa vya kupima virusi vya Corona na vile vya kujikinga, ametoa hadhari kuwa lazima ipitie Wizara ya Afya ili ipimwe kama ni salama kwa matumizi, kabla ya kukubalika kutumika nchini.