Back to top

WAFANYABIASHARA MBOZI WAGOMA KUFUNGUA SOKO

24 February 2026
Share

Wafanyabiashara wadogo zaidi ya mia moja katika soko la Ichenjezya, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, wamegoma kufungua vibanda vyao kwa muda usiojulikana kupinga hatua ya Halmashauri kuwafungia wenzao. 

Mgogoro huo umechochewa na madai ya malimbikizo ya kodi ya pango kuanzia mwaka 2021 hadi 2026, ambapo wafanyabiashara wanatakiwa kulipa malipo ya Shilingi 15,000 kwa mwezi kwa vibanda na Shilingi 5,000 kwa vizimba kwa mkupuo.

Uongozi wa soko hilo umeeleza kuwa jitihada za kukutana na mamlaka za serikali ngazi ya wilaya ili kuomba kulegeza utaratibu huo zimegonga mwamba, hali iliyowaacha bila ufumbuzi wa kudumu. 

Wafanyabiashara hao wamesimama kidete wakidai kuwa utaratibu wa kulipa madeni hayo kwa mkupuo mmoja unawaumiza kiuchumi na kushindwa kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, ameshikilia msimamo wa serikali kwa kuagiza Halmashauri kuhakikisha madeni yote ya nyuma yanalipwa kabla ya wafanyabiashara kupewa mikataba mipya. 

Hata hivyo, ametoa agizo la kibinadamu kwa wafanyabiashara wenye bidhaa zinazoharibika haraka kuruhusiwa kuzichukua, huku akisisitiza kuwa vibanda hivyo vitabaki wazi mpaka pale wahusika watakapokamilisha malipo ya kodi wanazodaiwa.