Back to top

Wagonjwa wa COVID 19,wapungua nchini-Majaliwa. 

24 May 2020
Share

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema maabukizi ya virusi vya Corona yamepungua nchini ambapo  katika hospitali ya Amana yupo mgonjwa mmoja, Mloganzila yupo mmoja, Temeke hakuna mgonjwa aliyethibitishwa, Kairuki hakuna mgonjwa, Rabiansia hakuna mgonjwa, Regency hakuna mgonjwa, Aga Khan yuko mgonjwa mmoja, Lulanzi Kibaha wapo wagonjwa 16 na Dodoma Mkonze mpaka leo asubuhi wapo wagonjwa tatu.

Hayo yamesemwa leo  na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akizungumza na waumini wa dini ya kiislam mara baada ya kumaliza kuswali sala ya Eid El Fitri katika Msikiti wa Gaddafi, jijini Dodoma. 

Aidha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais  Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza waislam kote nchini kwa kumaliza mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na anawashukuru kwa namna walivyoshiriki kuliombea Taifa hasa  katika kipindi hiki cha ugonjwa wa COVID-19.
 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania wote kwa ujumla waendelee kushirikiana katika kulifanya Taifa liwe la amani na utulivu. “Dini zetu zinatutaka kila mmoja aendelee kuomba, nchi hii imekuwa na utulivu sana na mfano duniani kwa nchi zinazotaka amani.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema wananchi watakiwa waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa COVID-19, ambapo amewasisitiza wasiwe na hofu na waendelee kufanya kazi kwa bidii.