Back to top

Wahamiaji haramu wahukumiwa kifungo cha miezi sita Iringa.

15 February 2019
Share

Mahakama ya Hakimu Mkazi wa wilaya ya Iringa imewahukumu kifungo cha miezi sita kila mmoja wahamiaji haramu kwa kosa la kuingia nchini bila vibali huku wahamiaji wengine saba raia wa Ethiopia na mmoja Mzambia kesi yao ikiahirishwa baada ya kukosekana mkalimani wa lugha wanazozungumza.

Akiwasomea mashitaka mbele ya hakimu mfawidhi wa Mahakama ya mkoa wa Iringa Liadi Chamshama mwendesha mashitaka wa uhamiaji mkoa wa Iringa Lameck Chiloli amesema mshitakiwa wa kesi namba 10 ya mwaka 2019 Samuel Kamani raia wa Kenya alikamatwa katika kituo cha mabasi mjini Iringa na kushitakiwa kwa kosa la kuwepo nchini bila kuwa na hati ya kusafiria wala kibali chochote kinachomruhusu kuwepo nchini.

Mshitakiwa mwingine katika kesi namba 8 ya mwaka 2019 John Kailanga raia wa Uganda alikamatwa Januari 20 mwaka huu akiwa nchini bila kibali kosa ambalo ni kinyume na sheria namba 45 kifungu cha kwanza (i) na cha pili chini ya marekebisho ya mwaka 2016.

Kwa mujibu wa kamanda wa jeshi la uhamiaji mkoani hapa Tununasia Adam watuhumiwa wote wamekamatwa katika operesheni ya kusaka wahamiaji wasio na vibali iliyofanyika kati ya mwezi wa kumi na mbili mwaka jana na mwezi wa kwanza mwaka huu.