
Takribani wahamiaji na wakimbizi 400 wamefanya maandamano katika bandari ya kisiwa cha Rhodes, wakishinikiza kuhamishiwa katika maeneo mengine nchini Ugiriki na kutatiza usafiri bandarini hapo.
Wengi wa waandamanaji hao waliokuwa wakipinga hali zao duni, ni wale waliookolewa baada ya kuvuka bahari hatari ya Mediterania kisha kusafirishwa hadi katika kisiwa hicho kwa ajili ya kushughulikiwa maombi yao ya ukimbizi.
Mazungumzo yanaendelea kati ya wahamiaji hao na idara ya polisi kisiwani humo.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi wahamiaji na wakimbizi 10,790 waliwalisili Ugiriki katika miezi minane ya kwanza 2023, hii ikiwa ni mara dufu ya takwimu za mwaka uliopita ambapo takriban watu 5,216 waliingia nchini humo.
