
Kundi la wanafunzi wasiopungua 39 nchini Korea Kusini, wameishtaki Serikali ya nchi hiyo, wakilalamikia muda wa mtihani kumalizika mapema zaidi, tofauti na muda halisi uliokuwa umepangwa ambao ulionyesha kuwa zilibaki sekunde 90, ndipo mtihani huo umalizike.
.
Mtihani huo wa udahili wa kujiunga na vyuo vikuu, unaojulikana kama Suneung, ambao hujumuisha masomo mbalimbali, unatajwa kuwa ni moja mtihani mgumu zaidi duniani na wenye viwango vya juu sana, na hufanyika kwa muda wa masaa 8 mfululizo.
.
Akizungumza na vyombo vya habari, Wakili wa wanafunzi hao, Kim Woo-suk, alisema kuwa hali hiyo iliwaathiri wanafunzi katika mitihani iliyokuwa imesalia na kwamba Mamlaka ya elimu nchini humo haikuomba msamaha juu ya sintofahamu hiyo, huku Shirika la Utangazaji la nchini humo likiwanukuu baadhi ya Maofisa waliosema kuwa Msimamizi Mkuu wa mtihani alisoma vibaya wakati.
.
Imeelezwa kuwa, kutokana na umuhimu wa mtihani huo baadhi ya hatua huchukuliwa, ikiwemo kufunga anga ya nchi na kuchelewesha kufunguliwa kwa soko la hisa, ili kuleta utulivu utakaowafanya wanafunzi kuongeza umakini zaidi katika mitihani hiyo.
