Back to top

Wakazi Dar watakiwa kuendelea kuchukua tahadhari kujikinga na Corona.

21 May 2020
Share

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt.Rashid Mfaume amewataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam waendelee kuchukua hatua za tahadhari ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Ametoa wito wakati akipokea msaada wa barakoa elfu kumi na saba na mia tano na lita mia saba za vipukusi au vitakasa mikono kutoka kwa shirika lisilo la kiserikali la Medipeace linalohusika na mradi wa Mama na Mtoto katika mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema licha ya elimu inayotolewa na wataalam wa afya juu  ya namna ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona, shirika hilo linawahamasisha wananchi wasibweteke katika kipindi hiki, ili kuutokomeza ugonjwa huo nchini.

Dkt.Mfaume amesema msaada huo utaelekezwa katika hospitali za Sinza ,Vijibweni, Rangi Tatu, vituo vya afya vya Kimara, Tandale, Mbezi, Round Table, Kimbiji, Buguruni na zahanati za Tegeta na Bunju.

Mwakilishi Mkazi wa shirika hilo Sukyung Kim amesema limekuwa likishirikiana na wizara za Afya na Tamisemi katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika mkoa wa Dar es Salaam.