
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw.Paul Chacha, amewaamuru walimu wawili wa shule ya Msingi ya Mabatini, iliyopo Manispaa ya Tabora, Juma Mahundi na Rose Mgaya, waliogoma kuripoti katika vituo vyao vipya vya kazi, baada ya kupatiwa uhamisho mnamo Mei 06, 2024, kuripoti mara moja katika vituo hivyo, kabla ya serikali haijawachukulia hatua za kisheria.
.
Mwalimu Rose Mgaya, alihamishiwa katika Shule ya Msingi ya Farm Nyamwezi na Mwalimu Juma Mahundi alihamishiwa katika Shule ya Msingi ya Ndevelwa, zilizopo ndani ya Manispaa ya Tabora, lakini waligoma kuripoti, ambapo wanadaiwa kuwa walikuwa wakiwatishia viongozi wao akiwemo Mkuu wa Shule na Afisa Elimu kuwa wana ndugu TAMISEMI.
.
Kufuatia sintofahamu hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw.Paul Chacha, amesema serikali haitaendelea kuwavumilia watumishi wanaochagua mazingira ya kazi na kudumaza juhudi za serikali kutoa elimu bora kwa wanafunzi wa maeneo ya pembezoni.
