Back to top

WALIOFARIKI KWA MAFURIKO WAFIKIA 100 SOMALIA

25 November 2023
Share

Baraza la Mawaziri la Somalia, limesema idadi ya waliofariki dunia kutokana na mafuriko nchini Somalia, inakaribia mia moja ambao ni miongoni mwa takribani watu milioni mbili walioathirika na mafuriko yanayoendelea.

Limesema zaidi ya watu laki moja na elfu kumi na tatu wamepoteza makazi yao kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo.

Somalia, kama nchi nyingine katika Pembe ya Afrika, inakabiliwa na mvua kubwa na mafuriko, wakati huu ikiwa imetoka kushuhudia hali mbaya kutokana na ukame uliowaweka mamilioni ya raia kwenye hatari ya kufa kutokana na baa la njaa.

Mapema mwezi huu serikali ilitangaza hali ya hatari kutokana na mafuriko, ambayo yamesababisha watu zaidi ya laki 7 kupoteza makazi, mashamba na miundombinu mingine.

Mvua zinazoendelea kunyesha nchini humo zinahusishwa na hali ya hewa ya El Nino, ambayo inatarajiwa kudumu hadi angalau mwezi April mwakani.