Back to top

WAMILIKI WA SAULI, NEW FORCE WATAKIWA KUTOA MAELEZO

02 April 2024
Share

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imewataka wamiliki wa mabasi ya Sauli na New Force yaliyosababisha ajali mnamo Machi 28, 2024, majira ya saa 09:42 Alfajiri, ambapo magari matatu (yakiwemo ya Sauli na New Force) yaligongana katika eneo la Mashamba ya Mpunga wilayani Kibaha, Mkoani Pwani katika barabara ya Morogoro, na kusababisha vifo vya watu wawili (2), majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali, kutoa maelezo kwa maandishi kabla ya kuchukuliwa hatua za kiudhibiti.
.
LATRA imesema, kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, ajali hiyo imetokana na uzembe wa dereva wa basi namba T 668 DTF Scania mali ya Mwalabhila Sauli kutaka kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, huku madhara ya ajali hiyo yakisababishwa na uzembe wa dereva wa basi namba T 175 DZU linalomilikiwa na kampuni ya New Force kushindwa kuacha umbali wa gari lililokuwa mbele yake kama inavyopaswa.
.
Pia, kulingana na taarifa za Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS), tarehe ya tukio magari namba T 175 DZU na T 668 DTF yalianza safari kutoka Dar es salam kwa pamoja saa 8:44 usiku, ambapo kwa mujibu wa leseni walizopewa, mabasi hayo yalipaswa kuanza safari saa 9:00 na saa 10:30 alfajiri, mtawalia, huku uchunguzi zaidi kwenye mifumo ya Mamlaka ukionesha kuwa madereva wa mabasi hayo wamesajiliwa kwenye mifumo ya Mamlaka lakini hawakutumia vitufe vya utambulisho (i-Button).