Back to top

Wanafunzi shule ya Mitambo waondokana na adha ya kusomea mikoroshoni.

16 May 2018
Share

Wanafunzi wa shule ya msingi Mitambo kata ya Mitambo halmashauri ya wilaya ya Mtwara,waliokuwa wakisomea chini ya mikorosho na kwenye mabanda yaliyoezekwa kwa makuti,wameondokana na adha hiyo,baada ya serikali na wadau wengine wa elimu kuchangia ujenzi wa madarasa  matano na ofisi moja ya mwalimu.

Akizungumza na ITV mwalimu mkuu wa shule hiyo ya mitambo Rashid Chalido amesema, ujenzi kwa madarasa hayo mapya, kati yake mawili yamekwisha kamilika na kuanza kutumika, umeboresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya kujifunzia na kufanya tatizo la utoro wa wanafunzi shuleni hapo kupungua,ambapo sasa mahudhurio yamepanda toka asilimia 65 hadi asilimia 85.

Hata hivyo, mmoja wa mafundi wanaohusika na ujenzi wa madarasa hayo Issa Mohamed amesema, changamoto kubwa inayowakabila katika ujenzi huo ni upatikanaji wa maji, huku mwenyekiti wa kijiji hicho cha Mitambo Salum Akola akikiri tatizo hilo ni kubwa na la muda mrefu, ambapo wakazi wake hulazimika kutumia maji yasiyo salama ya kwenye mabwawa, lakini akabainisha, uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara umeahidi kukamilisha kisima kilichojengwa, ili kianze kutoa maji hivi karibuni.