
Wananchi wa Mahenge katika Halmashauri ya Wilayani ya Ulanga, Mkoani Morogoro wametakiwa kuchangamkia fursa zinazotolewa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ili waweze kujikwamua kutoka katika windi la umasikini kwa kuongeza kipato na kukuza uchumi.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Bw. Peter Nambunga, alisema hayo katika program maalum ya elimu ya fedha kwa umma iliyotolewa kwa wananchi wa Mahenge na wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na washirika wa sekta ya fedha nchini.
Bw. Nambunga aliongeza kuwa wananchi wa Mahenge na Tanzania, kwa ujumla wanatakiwa kuzitumia fursa zaidi ya 72 zinazotolewa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, katika kuendeleza shughuli zao mbalimbali za uzallishaji mali ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla na kusaidia kupeleka mbele gurudumu la maendeleo.
Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii huyo aliwataka wananchi wa Mahenge na Halmashauri nzima ya Ulanga kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha ili kuwaepusha na uhitaji wa kutafuta mikopo isiyo ya lazima na kwa kufanya hivyo itakuwa njia mojawapo ya kuepukana na mikopo ya kausha damu.
Awali akizungumza katika program hiyo, Mratibu wa Mifuko na Program za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kutoka Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bw. Samwell Shikona, alisema kuna fursa mbalimbali za kuwakomboa wananchi kiuchumi zikiwemo mikopo kwa wakulima ambayo ina masharti nafuu, lakini kuna mikopo nafuu inayotolewa kwa wakulima ambao wana umri kati ya miaka 18 hadi 40 ambayo haina masharti yoyote.