
Hekari zaidi ya 10 za mazao ya wakulima wa wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro zimeharibiwa na jeshi la Polisi kwa madai kuwa zimeoteshwa kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya matumizi ya mafunzo hatua ambayo imelalamikiwa na wananchi na viongozi wa eneo hilo.
Wakizungumzia suala hilo wakulima hao pamoja na kukiri kuwa eneo walilootesha mazao hayo lina mgogoro wamesema walishakubaliana kulitumia kwa muda wakati huu ambao halitumiki lakini wanashangaa kuona mazao yao yanaharibiwa.
Mbunge wa jimbo la Siha Dkt. Godwin Mollel amesema suala hilo lilishafikishwa kwa viongozi wa ngazi za juu na lilikuwa linaendelea kutafutiwa ufumbuzi kwa njia ya amani bila kuleta athari na kwamba kimsingi hakukuwa na sababu ya kuharibu mazao ya wananchi .
Akizungumza kwa njia ya simu Kamishina Mwandaizi Msaidizi wa polisi Ramadhani Mungi amesema eneo hilo lipo kwa ajili ya mafunzo na kamwe sio la kilimo na kwamba kilimo na mafunzo ya kijeshi haviwezi kwenda sambamba.