Wananchi katika kijiji cha Utengule kata ya Mambwenkoswe wilayani Kalambo mkoani Rukwa wamelazimika kuchangishana fedha na kujenga kivuko cha miti katika mto Mlenje baada ya mto huo kujaa maji wakati wa masika na kusababisha wanafunzi pamoja na wakazi wengine kushindwa kuvuka na hivyo kukatika kwa mawasiliano na kuiomba serikali kupitia wakala wa barabara vijijini na mijini TARURA kujenga daraja la kudumu.
Wakiongea katika nyakati tofauti, wananchi kijijini hapo wamesema serikali haina budi kuwasaidia kujenga kivuko imara kwani kilichopo si salama kwa maisha yao kutokana na kujengwa kwa miti ambapo mwaka jana serikali ya kijiji husika ililazimika kuifunga shule ya msingi ili kuokoa maisha ya watoto.
Meneja wa barabara za vijijini na mijini TARURA wilayani Kalambo Japhet Elvas, amesema serikali imetenga bajeti kwa mwaka 2020 /21 kwa ajili ya ujenzi kwa kivuko hicho na kuwasihi wananchi kuwa wavumilivu wakati suala lao likishughulikiwa na huku kaimu mkurungezi wa halmashauri hiyo Magreth Kakoyo akiwataka wananchi kuwa makini na watoto wao ili wasivuke kwenye mto huo pindi maji yanapojaa.