Back to top

Wananchi waingiwa na hofu ya tembo Same mkoani Kilimanjaro.

15 May 2019
Share

Wananchi wa vijiji vya Makanya, Hedaru, Saweni, Bangalala na Kisiwani wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro, wamejawa na hofu kubwa kufuatia wanyama aina ya Tembo kuonekana mara kwa mara katika makazi yao na kufanya uharibifu wa mazao, vifo na kujeruhi huku wananchi wakiishi kwa wasiwasi hasa wanapokuwa mashambani kwa msimu huu wa kilimo.

ITV imetembelea katika baadhi ya vijiji hivyo ikiwemo kijiji cha Saweni na Vumari ambapo wananchi hao wamesema tangu kuanzishwa kwa vijiji hivyo hawakuwahi kuona Tembo katika mazingira hayo hali ambayo inapelekea hofu kubwa kwao.

Aidha wananchi hao wameiomba serikali kuona namna ya kutoa elimu ya wanyama hao kwa upana zaidi kwani baadhi yao hawajui madhara ya wanyama hao hasa wanapo chokozwa kwa kufukuzwa na kupigiwa kelele za madebe.

Kufuatia kadhia hiyo mashirika yanayo husika na uhifadhi wa mazingira wamelazimika kutoa mafunzo ya uhifadhi na jinsi ya kukabiliana na wanyama hao waharibifu katika vijiji sita vya wilaya hiyo ya Same.