
Baadhi ya wafanyabiashara katika halmashauri ya wilaya Momba mkoani Songwe wamesema Operesheni ya kupanua wigo wa kodi inayofanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kuzifikia Kata zote za mkoa huo, itasaidia kujenga uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na maendeleo ya uchumi.
Wakati wa Operesheni hiyo iliyoanzia katika Kata ya Chitete makao makuu ya wilaya Momba, wafanyabiashara wamekiri kuwa baada ya kuelimishwa kuhusu taratibu za ulipaji mapato, wamegundua kuwa tatizo la makadirio makubwa ya kodi linachangiwa na ukosefu wa elimu sahihi ya kudhibiti mahesabu ya kibenki.
Wamesema, wengi wa wafanyabiashara wanafanya mizunguko ya fedha ili kupata sifa za kunufaika na mikopo mbalimbali bila kujua kuwa makadirio ya kodi huzingatia hesabu za mzunguko Huo bila kujali pesa iliyotumika ni ya mkopo ama vinginevyo.
Ili kujenga uelewa wa kutosha kwa wafanyabiashara hao, TRA imeanza kupaza sauti ya elimu kwa kila Kata, zoezi linaloambatana na utoaji wa Leseni pamoja namba za utambulisho wa mlipakodi (TIN) zoezi lililoanzia wilayani Momba, likiungwa mkono na Mkuu wa wilaya hiyo. Fakie Lulandala.