
Wauguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya ziwa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza wameviomba vyombo vya dola, likiwemo Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kali za kisheria baadhi ya watu wanaowashambulia na kuwapiga wakiwa kazini kwani hali hiyo inavunja moyo wa kizalendo wa kujituma zaidi wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Ombi la wauguzi wa hospitali hiyo ya Rufaa Bugando linafuatia tukio la muuguzi wa hospitali hiyo aliyekuwa zamu ya mchana kushambuliwa na ndugu wa mgonjwa aliyekuwa amelazwa wodi namba 8, baada ya kukuta mgonjwa wao amefariki dunia Januari mwaka huu, ambapo wauguzi hao kupitia kwa muuguzi wa hosptiali hiyo Eliael Msuya wameomba taratibu za kisheria zichukuliwe dhidi ya raia wanaowapiga wauguzi wakiwa kazini ili kutowavunja moyo wa kufanya kazi, kwani kazi ya uuguzi ni kazi ya wito inayohitaji kujitoa zaidi na kutanguliza ubinadamu mbele kuliko maslahi binafsi.
Naibu Mkurugenzi wa huduma za afya wa hospitali hiyo Dk. Bahati Wajanga amesema licha ya wauguzi kukabiliwa na changamoto mbalimbali,zikiwemo za kupigwa na baadhi ya ndugu wa wagonjwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kutolipwa stahiki zao mbalimbali kwa wakati, ameahidi kuzifanyia kazi ili zisiweze kujitokeza tena, huku akiwapongeza kwa kukabiliana na changamoto bila kukata tamaa na kuwaomba wasirudi nyuma kwani uongozi wa hospitali hiyo uko pamoja nao.
Mkurugenzi wa huduma za upasuaji hospitalini hapo Sista Dk. Alicia Masenga pamoja na Katibu wa Chama cha Wauguzi ( TANNA ) hosptali ya Rufaa Bugando Yunis kitula wanaeleza walivyojipanga kutoa huduma bora za afya kwa uaminifu na weledi wa hali ya juu.