
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto Mh. Ummy Mwalimu amesema serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi ambazo zinasaidia kuibua na kuthamini uwezo wa wanawake nchini kwa lengo la kujenga jamii inayoheshimu haki, ustawi na maendeleo ya nchi kwa wanawake wanao onyesha nia na udhubutu wa kutenda jambo.
Mh.Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo ya serikali jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo ya Malikia wa nguvu Mwaka 2018 iliyondaliwa na uongozi wa Clouds Media Group na kuwataka wanawake kupambana na changamoto ya udhubutu wa kufanya jambo lolote la maendeleo ili kuhakikisha shabaha ya 50 kwa 50 inafikiwa kwa asilimia mia moja ifikapo mwaka 2025.

Katika hafla ya Malkia wa nguvu kwa Mwaka 2018 jumla ya wanawake 13 walioshiriki moja kwa moja kuibua miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kuwapatia kipato walipewa tuzo,pamoja na kutambua pia wanawake waliochangia mafanikio katika taaluma mbalimbali ikiwemo tansia ya habari kwa zaidi ya miaka 20 hapa nchini na safari hii tuzo hiyo ya heshima akapatiwa Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/Radio One, Joyce Mhavile huku tuzo ya jumla ya heshima ikienda kwa Mama Maria Kamu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Bi. Sofia Mjema amesema serikali ya Ilala itasaidia kwa kila uwezo ilionao kwa wanawake wote wabunifu waliobuni njia halali za kujipatia kipato na kutunukiwa tuzo ya Malkia wa nguvu mwaka 2018.
