Back to top

Wasichana zaidi 50 waliotaka kukeketwa na kuozeshwa waepushwa

30 September 2018
Share

Wasichana zaidi ya hamsini wa jamii ya wafugaji kutoka Wilaya za Monduli na Simanjiro wameepushwa wakati wazazi wao wakiwa kwenye harakati za kutaka kuwafanyia mila ya ukeketaji na baadhi yao kuozeshwa wakiwa katika umri mdogo unaostahili kuwa shuleni.

Wasichana hao waliookolewa na kuhifadhiwa kwenye kambi maalum na kupatiwa huduma mbalimbali muhimu zikiwemo za  kujiendeleza na elimu wanasema bado nguvu kubwa ya elimu inahitajika kuelekezwa kwa wazazi wa jamii yao ili waweze kutambua athari ya mila hizo kwa maendeleo ya mtoto wa kike.

Shirika linalojishughulisha na utetezi wa haki za wanawake, afya ya uzazi na mazingira ndani ya jamii hiyo la HIMS ndilo lililowaokoa wasichana hao katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka jana na kuwahifadhi wakishirikiana na watetezi wengine waliopo ndani ya jamii hiyo.

Akizungumza katika ziara ya maafisa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu kuona hali halisi ya mila hizo katika wilaya hizo zinazokaliwa na wafugaji, Afisa Mawasiliano wa shirika hilo, Bwana WARREN BRIGHT amesema bado mila hizo ni tatizo linalohitajii ushirikiano wa wadau wote wa maendeleo kuzitokomeza.