
Siku moja baada ya ITV kurusha habari ya uwepo wa tope mithili ya volkano Kunduchi jijini Dar es Salaam jopo la wataalamu kutoka Idara ya Geolojia iliyopo chini ya shule kuu ya migodi na Geosayansi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamefika eneo hilo na kubaini kupasuka kwa mwamba huku wakichukua sampuli ya tope hilo kwa uchunguzi zaidi.
Jopo hilo likiongozwa na Mkuu wa Idara Dk. Elisante Mshiu lilifika majira ya asubuhi na kuanza uchunguzi wa mlipuko huo wakishirikiana na vikosi vya polisi wilaya ya Kawe chini ya ASP Masota na kubaini athari kubwa ambazo zimewahi kutokea bila kuripotiwa ikiwemo nyumba kupata nyufa kubomoka na nyingine kuwahi kuzama kabisa.
Aidha Dk. Mshiu sambamba na kuchunguza tope hilo katika maabara pia anaeleza nia ya kufanya uchunguzi wa kubaini mipaka ya mpasuko hai wa mwamba huo anaoueleza kuchagizwa na uchimbaji kokoto na Gypsum katika ukanda huo ili kuepuka madhara zaidi.