
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, maliasili na Mifugo kutoka Zanzibar, Mhe.Shamata Saame amewataka wataalam wa Sekta ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha wanachukua takwimu sahihi wakati wa kukusanya taarifa za kitafiti ili ziweze kuisaidia Serikali katika kupanga mipango yake.
Waziri Shaame ameyasema hayo wakati akifunga Kongamano la 46 la Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Mkutano Mkuu wa 47 wa Mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) lililofanyika kwenye Ukumbi wa Olasit Garden, Arusha Oktoba 27, 2023.
"Takwimu sahihi kuhusu taarifa za mifugo na uvuvi zitasaidia kutunga sera, kunyoosha maono, fikra na miongozo ya ilani ya chama cha mapinduzi kuweza kufikia malengo ya kuwainua wananchi kupata mafanikio kwa haraka," alisema
Ameongeza kwa kusema kuwa Serikali inawategemea sana wataam na hivyo watumie vizuri teknolojia walizonazo ili zikaboreshe tasnia nzima ya ufugaji ili kupata maendeleo.


“Wizara na Wadau wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa pamoja lazima tutambue kuwa huu ni wakati mwafaka wa kufanya mapinduzi makubwa katika minyororo ya thamani ya mifugo na samaki ili kukidhi mahitaji ya chakula na lishe bora kwa Wananchi na masoko yanayotuzunguka” Alisema Mhe. Shaame
Ameendelea kwa kuwahimiza Wafugaji na wazalishaji kuwekeza katika teknolojia za kisasa na vitendea kazi sahihi vitakavyoongeza uzalishaji katika kilimo, mifugo na sekta ya Uvuvi na hivyo Wizara, itaendelea kuhakikisha kuwa mazingira bora ya kufuga, kusindika na kufanya biashara ya mifugo na uvuvi yanazidi kuwa bora kwa watengenezaji wa vyakula vya mifugo na samaki.
Ameongeza kuwa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo inaunga mkono jitihada za vyama vya hiari vya kitaaluma , hivyo TSAP iendelee kujitangaza ili kuongeza mashirikiano na wataalamu walioko Zanzibar ili kuendelea kupata wanachama wengi.
Naye Naibu Katibu Mkuu amewataka wataalam kuweka bidii katika kujiendeleza kutaaluma ili kuongeza ujuzi na ufanisi zaidi katika kazi zao na kuweza kutengeneza mfumo utakaohifadhi taarifa za wataalam wote wa mifugo nchini ili kujua umma uliopo ni asilimia ngapi ya wataalam walioko huko nje.
Pia amewataka wataalam kuwa chachu ya kuhamasisha wafugaji kulima, kuhifadhi malisho na kutengeneza vyanzo mbadala vya maji kwa mwaka mzima ili kupunguza idadi kubwa ya vifo vya wanyama vinavyotokea kipindi cha kiangazi.
