Back to top

WATAFITI WATAKIWA KUSAIDIA SEKTA YA MIFUGO

21 July 2022
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Mashimba Ndaki amewataka Watafiti wa Mifugo nchini kuhakikisha, wanafanya tafiti zitakazosaidia Sekta ya Mifugo kuzalisha kwa tija na kuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa.

Waziri Ndaki ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Mifugo uliofanyika Jijini Dodoma.

Akiongea na wadau hao, Waziri Ndaki amesema wafugaji wengi nchini bado wanafuga kienyeji  na kupelekea sekta ya mifugo kutokuwa na tija kubwa, hivyo ni wakati sasa watafiti wasaidie kutatua changamoto hiyo. 

"Kama tutaendelea kufuga kama tunavyofuga leo kwa kuswaga Ng'ombe, baada ya miaka kumi ijayo tutaleta shida kwenye nchi hii, kwa sababu maeneo ya malisho yamepungua, hivyo watafiti watusaidie kuja na majibu yanayolenga kutatua changamoto hii, tuone namna gani tutakabiliana na jambo hili",Amesema

Ameongeza kwa kusema kuwa kwa upande wa Wizara kuanzia mwaka huu wa fedha  wamejipanga kufanya kampeni kubwa ya kuwaelimisha wafugaji nchi nzima kuhusu ufugaji bora na wenye tija.  

"Tutaanza kutoa elimu  mwaka huu kuwaelimisha wafugaji kuhusu ufugaji bora na tutaendelea mpaka ujumbe huu wa kufuga kwa tija uwe umefika kwa wafugaji wote nchini", Amefafanua

Aliendelea kusema kuwa Wizara imetenga bajeti kwa ajili ya kuelimisha wafugaji kuhusu malisho ya mifugo na mabadiliko ya tabia nchi ili wabadilike kutoka kufuga kiasili na kufanya ufugaji wa kibiashara.

Kuhusu uhaba wa Wataalamu wa Ugani, Waziri Ndaki alisema mwaka huu serikali itaajiri Maafisa Ugani zaidi ya 300 ili kupunguza changamoto hiyo huku akiongeza kuwa watanunua  pikipiki zaidi ya 1000 kwa ajili ya kuwawezesha maafisa hao kuwahudumia wafugaji kwa urahisi.

Naye, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo), Dkt.Charles Mhina alisema kuwa maendeleo ya sekta ya mifugo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na sekta binafsi hivyo Serikali itaendelea kuweke Mazingira mazuri kwa wadau hao ili sekta hiyo iweze kuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa.