
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele katika utunzaji wa misitu kwa kutekeleza azma ya uhifadhi na uendelezaji misitu kwa vitendo.
Amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) imeendelea kuratibu utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya upandaji na utunzaji wa miti inayotekelezwa nchini kwa kila Halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.
"Katika kipindi cha mwaka 2020/21, Halmashauri 27 kati ya 184 zilivuka lengo la kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka ambapo idadi ya miti 202,923,907 ilipandwa na miti 165,501,119 ilistawi, ambayo ni sawa na asilimia 81.6"Mhe.Majaliwa.
Amesema hayo wakati akizindua zoezi la upandaji miti katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma. "Watanzania tuendelee kupanda na kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa miti na misitu kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu.

Amesema kuwa suala la upandaji wa miti na kuitunza ni la muhimu kwa ustawi wa mazingira ya Taifa kwani hatua hiyo inakwenda sambamba na uhimili wa mabadiliko ya tabia ya nchi na kuwezesha mazingira kuwa ya kijani na mandhari mazuri ya kuvutia.
"Ndege wa angani na wanyama wa porini wote wanategemea miti kwa chakula na wengine kwa makazi. Hata mifugo na binadamu tunategemea miti kwa chakula na mahitaji mengine"Mhe.Majaliwa
Ameongeza kuwa sekta ya misitu huchangia asilimia 45 ya mahitaji ya malighafi ya ujenzi, hulinda vyanzo vya maji na kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Mhe.Majaliwa amesema kwa kutambua umuhimu huo Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele katika utunzaji wa misitu na imekuwa ikitekeleza azma ya uhifadhi na uendelezaji misitu kwa vitendo.
"Tayari Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania imeshaanzisha mashamba makubwa ya miti"Mhe.Majaliwa
"Misitu huchangia kuinua pato la Taifa na pato la mtu mmoja mmoja, Serikali kwa kutambua hilo imeendelea kutekeleza mikakati ya kuwanufaisha wananchi wanaoishi jirani na misitu kupitia miradi ya ufugaji nyuki na miradi ya ufundi seramala"Mhe.Majaliwa
