Back to top

WATANZANIA WATAKIWA KUSHIRIKI KUDHIBITI UGONJWA WA KICHAA CHA MBWA

29 September 2022
Share

Watanzania wametakiwa kudhibiti ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambao takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 60,000 hufariki duniani kila mwaka huku wastani wa matukio ya majeraha kwa binadamu yanayotokana na kuumwa na mbwa ni 3,387 kila mwaka.

Senyamule amesema kuwa kwa mujibu wa repoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2017, ugonjwa wa kichaa cha mbwa husababisha wastani wa vifo vya binadamu 1,500 kila mwaka nchini Tanzania.

Takwimu zaidi zinaonesha kuwa watoto chini ya umri wa miaka 15 ndiyo hupatwa zaidi na madhara haya kwa kuwa na ukaribu na urafiki na mbwa.

Aidha, amesema kwa hapa Tanzania, kila mwaka kuna wastani wa matukio 2,030 ya mbwa wanaodhaniwa kuwa na kichaa. ‘’Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Afya za Wanyama Duniani (WOAH) na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) kwa pamoja yamekubaliana kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa ifikapo 2030. 

Mbali na hilo, amesema kuwa Tanzania ina mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa wa mwaka 2019. Lengo lake ni kudhibiti ugonjwa wa kichaa cha mbwa na hatimaye kuutokomeza kabisa ifikapo 2030. Pia, kuna Mpango Mkakati wa Afya Moja (2015-2020) unaotoa wajibu wa kila mmoja katika kudhibiti ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa njia ya chanjo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Senyamule wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya kichaa cha mbwa duniani yaliyofanyika kwenye eneo la mnadani kata ya Mpunguzi Septemba 28,2022 jijini Dodoma.

Aidha, Senyamule amepongeza jitihada zilizochukuliwa na Wizara uamuzi wa kidhibiti kichaa cha mbwa kwa mfumo wa kuendesha kampeni kwani njia hii inasaidia kufikisha ujumbe kwa watanzania wengi zaidi.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Hezron Nonga amesema kuwa kupitia kampeni hii watahakikisha mbwa wote wanachanjwa ili kuwakinga na ugonjwa huo. Hivyo ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha mbwa wao wanachanjwa katika kipindi hiki cha kampeni.

Prof. Nonga amesema kuwa hata baada ya kampeni hii kumalizika, uchanjaji wa mbwa utaendelea kufanyika kwa mwaka mzima.

Perez Rumolwa ambaye ni mfugaji wa mbwa alisema kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa huweza kusababisha kifo ikiwa mtu hatowahishwa hospitali.

Hapa nchini, kuna takribani mbwa milioni 4.5 na paka milioni 2 wanaofugwa kwa malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi, kusaidia kuchunga mifugo na uwindaji. Maadhimisho ya kilele cha wiki ya Kichaa cha Mbwa Duniani yanaongozwa na Kauli Mbiu inayosema “Kichaa cha Mbwa; Afya Moja, Vifo Sifuri”