Back to top

WATOTO 45 KUFANYIWA UPASUAJI WA MOYO

10 October 2023
Share

Watoto 45 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo, yakiwemo matundu kwenye moyo, na matatizo ya mishipa ya damu, kufanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalum, inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids lililopo nchini Marekani.

Kambi hiyo maalumu ya siku tano iliyoanza Oktoba 09, 2023 inatarajiwa kutoa matibabu ya upasuaji wa moyo wa tundu dogo, kwa kutumia mtambo wa 'cathlab' kwa watoto 25 na upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua kwa watoto 20.

Akizungumza na mwandishi wa habari Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto, wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela, alisema upande wa cathlab watoto 25 watapatiwa matibabu ya kuziba matundu mbalimbali yaliyopo katika kuta za moyo, pamoja na kufungua mishipa ya damu iliyobana inayopeleka damu kwenye mapafu na kwenye mwili.