Back to top

Watu 101 wakiwemo wafungwa 72 waambukizwa Corona Rwanda

30 June 2020
Share


Kwa mara nyingine tena Rwanda imetangaza rekodi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya Corona, baada ya watu 101 wakiwemo wafungwa 72 wa gereza la Ngoma Mashariki mwa Rwanda, kuthibitishwa kuambukizwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Covid 19 ndani ya saa 24 zilizopita, hii ndiyo rekodi kubwa zaidi kuwahi kutangazwa nchini humo, tangu mgonjwa wa kwanza abainike katika ardhi ya taifa hilo, taehe 14 Machi mwaka huu.

Miongoni mwa wagonjwa hao wapya, 72 ni wafungwa wa gereza la Ngoma lililopo wilayani Ngoma mashariki mwa Rwanda na inasemekana waliambukizwa baada ya kutengamana na watu walio karibu na mpaka wa Rusumo unaotenganisha Rwanda na Tanzania.

Kwa maana hiyo rekodi ya wagonjwa wa Corona nchini humo imepanda mara dufu na kufika wagonjwa 1001, huku waliopona wakiongezeka na kufika watu 443 ambao wako hospitali ni 556 vifo bado ni viwili.

Ikumbukwe huku idadi ya wagonjwa wa Corona ikizidi kuongezeka, baadhi ya mitaa iliyokutwa na maambukizi makubwa jijini Kigali katika siku za hivi karibuni, imewekwa karantini ili kuzuia kuenea Zaidi kwa virusi hivyo katika maeneo mengine ya mji mkuu wa Rwanda Kigali.

Ugonjwa huo ulipoanza kusambaa kwa kasi nchini humo, serikali ilipiga marufuku watu kutembelea wafungwa ili usienee magerezani na wengi wanahoji, imekuwaje wafungwa wakaambukizwa virusi hivyo na hali hawatembelewi? Yamkini hili likawa ni swali tata ambalo wengi wetu hatuwezi kulipatia majibu.