Back to top

Watu 4 wanaswa na meno ya Tembo 13 mkoani Mbeya

22 August 2019
Share


Watu wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya baada ya kukamatwa wakiwa na vipande 13 vya meno ya Tembo bila kuwa na kibali jambo ambalo linadaiwa kuwa ni kinyume cha sheria za nchi.

Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Ulrich Matei amesema watuhumiwa hao walikamatwa jana katika maeneo tofauti wilayani Chunya baada ya askari wa jeshi la polisi kufanya msako mkali wilayani humo.

Katika hatua nyingine kamanda Matei amesema kuwa mtu mmoja anayesadikiwa kuwa askari wa jeshi la wananchi kikosi cha 44 KJ mbalizi mkoani Mbeya, Fred Grayson amefariki dunia papo hapo baada ya gari alilokuwa akiendesha kugongana uso kwa uso na lori katika eneo la ZZK, nje kidogo ya jiji la Mbeya.

Kamanda Matei ametoa onyo kwa vijana wanafanya ujangili wa kuua wanyama hasa tembo ili wajipatie utajiri wa haraka, kuacha mara moja kwani jeshi la polisi halitawafumbia macho huku akiwataka madereva kuchukua tahadhari wanapojaribu kuyapita magari mengine barabarani hasa nyakati za usiku ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.