Back to top

Watu saba wamefariki katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam

16 April 2018
Share

Watu saba wamefariki katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bwana LAZARO MAMBOSASA  amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kubainisha kuwa watu sita wameangukiwa na kuta za nyumba na mmoja mwili wake umekutwa ukielea kwenye maji.

Kamanda MAMBOSASA amesema bado Polisi inaendelea kufanya tathmini na kueleza kuwa barabara mbali mbali zimefungwa kutokana kutopitika kwa sababu ya kujaa maji ikiwemo Barabara ya Morogo eneo la Jangwani.

Ametoa wito kuwataka wananchi wajiepushe na ukaidi pale wanapoamriwa na Askari Polisi kuwataka wasipite kwenye njia ambazo zimezuiwa, kwamba wasilazimishe kwani maji siyo ya kuyajaribu.

Kamanda MAMBOSASA pia ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwaangalia watoto wao wanaokwenda shule ambao wanalazimika kuvuka maeneo yanayopitiwa na mikondo ya maji na kutaka watoto wasindikizwe kwenye barabara zinazopitika kwa urahisi.