Back to top

Watu Wasiojulikana wafunga ofisi ya serikali ya mtaa Jijini Mwanza.

20 February 2021
Share

Zaidi ya wakazi 3,000 wa mtaa wa mwananchi kata ya Mahina jijini Mwanza kwa miezi miwili sasa, wamekuwa wakihangaika kupata huduma za kiserikali bila mafanikio, baada ya kundi la watu wasiojulikana kuifunga ofisi ya serikali ya mtaa huo kwa madai ya kutoridhishwa na hatua ya kurejeshwa kwa wajumbe wanne wa serikali ya mtaa waliotuhumiwa kwa ubadhirifu pamoja na kuenguliwa madarakani kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo baada ya kunyang’anywa kadi ya uanachama wa CCM.
.
ITV imeshuhudia mlango wa ofisi ya serikali ya mtaa wa mwananchi, ukiwa umefungwa kwa makufuli mawili, huku baadhi ya wananchi wakilalamikia hali hiyo wanayodai imewatesa kwa muda mrefu, sanjari na kuzorotesha shughuli za maendeleo yao.
.
Tangu kufungwa kwa ofisi ya serikali ya mtaa huo Januari 17, mwaka huu, hali ya ulinzi na usalama pia inadaiwa kuparanganyika .
.
Sekeseke la kufungwa kwa ofisi ya serikali ya mtaa wa mwananchi liliibuka baada ya kurejeshwa madarakani kwa wajumbe wanne ambao ni Emmanuel Lobuya, John Martine, Juma Sumuni na Dorothy Sekito waliokataliwa na wananchi kwenye mkutano mkuu wa mtaa huo novemba 17 mwaka jana.