
Watu wanne wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mwanza kwa tuhuma za mauaji ya askari wa jeshi la akiba Nickson Jumbura katika kisiwa cha Bezi kilichomo ndani ya ziwa Victoria wilayani Ilemela baada ya kumshambulia kwa kutumia silaha za jadi wakati akitekeleza majukumu yake.
Marehemu Jumbura mkazi wa Kibara wilaya ya Bunda mkoani Mara, kabla ya kifo chake alikimbilia ziwani ili kujiokoa lakini watuhumiwa walimfuata na kuendelea kumshambulia na hatimaye kumzamisha majini kitendo kilichosababisha kifo chake.
Pia kamanda Muliro amesema jeshi la polisi mkoani humo limekamata transforma moja mali ya shirika la umeme nchini (TANESCO ) iliyoibwa wilayani Sengerema na kusafirishwa hadi eneo la Mwaloni Kirumba Mwanza, ambapo sambamba na tukio hilo watuhumiwa wengine 12 wanaojihusisha na utengenezaji, uuzaji na unywaji wa pombe haramu ya gongo kadhalika wametiwa mbaroni.
Kamanda huyo wa polisi mkoa wa Mwanza, ametoa onyo kwa baadhi ya wananchi wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu na wanaojichukulia sheria mkononi kuacha mara moja na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
