
Mahakama Kuu Kanda ya Iringa imewahukumu washtakiwa watatu Elias Jackson Mwenda (31) Hussein Khamis (31) na Orestus Mbawala (51) wakazi wa mkoa wa Mbeya kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya James Kaengesa mwendesha pikipiki mkazi wa mji wa Makambako mkoani Njombe.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Dk. John Utamwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi amesema tukio hilo lilitokea Juni mwaka 2016 mnamo saa mbili usiku ambapo marehemu ambaye alikuwa dereva wa bodaboda aliyokuwa akiimiliki,alikodiwa na moja ya washtakiwa hao na alipofika eneo la Mashujaa aliambiwa asimame na mshtakiwa huyo ambaye alikuwa amepakiwa kwenye bodaboda hiyo na baada ya kufanya hivyo washtakiwa wengine wakajitokeza na kumnyonga.
Amesema washtakiwa hao Baada ya kumnyonga walimtupa kwenye shamba la mahindi na kutoweka na pikipiki kuelekea mkoani Mbeya ambapo walikamatwa eneo la Rujewa wilaya ya Mbarali wakiwa na pikipiki hiyo.
Amesema hukumu hiyo kwa washtakiwa hao imetolewa kutokana na wao kwenda kinyume cha sheria ya makosa ya jinai chini ya kifungu cha 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.
Mawakili wa serikali ambao walikuwa upande wa Jamhuri na wakiwakilishwa na Matiku Nyangero na Andrew Mandwa wameiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya 2019 kwakuwa adhabu ya mauaji ya kukusudia ni moja tu ya kunyongwa hadi kufa.
