Back to top

WAWEKEZAJI WAZAWA WAHIMIZWA KUWEKEZA SEKTA YA MIFUGO

26 August 2022
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Mashimba Ndaki amewahimiza wawekeza kutoka Sekta binafsi nchini kuwekeza katika sekta ya mifugo kwa sababu kuna fursa kubwa ya kukuza mitaji yao na kupata faida.

Ametoa wito huo alipotembelea na kukagua maendeleo ya kiwanda cha kuchakata maziwa na chakula cha mifugo cha Kahama Fresh kilichopo Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera.

Waziri Ndaki amewahimiza wawekezaji wa sekta binafsi kuwekeza katika sekta ya mifugo nchini kwa sababu inawezekana  akitolea mfano muwekezaji huyo wa Kahama Fresh ambaye alianza uwekezaji katika shamba alilopewa na serikali na mpaka sasa amefungua kiwanda cha kuchakata maziwa na chakula cha mifugo.

Ameongeza kuwa wawekezaji hao binafsi wakiwekeza katika sekta ya mifugo na kufanya ufugaji wa kibiashara watasaidia kuongeza fursa za ajira kwa wananchi lakini pia watakuza pato la taifa.

Aidha, amesisitiza kuwa kupitia uwekezaji wao watasaidia Wafugaji wengine ambao wanafanya ufugaji wa kujikimu kujifunza kupitia kwao na kufanya ufugaji wenye tija kubwa zaidi.

Kwa upande wake Mwekezaji wa Kiwanda cha Kahama Fresh, Josam Mtangeki amesema kuwa wamekuwa wakipata changamoto ya maji na chakula cha mifugo hasa wakati wa kiangazi hivyo aliiomba Wizara kumuongezea eneo la lisilopungua hekta 2000 ili aweze kulima malisho kwa ajili ya mifugo yake na malisho mengine atawakopesha wafugaji wadogowadogo ambao wanamuuzia maziwa kwa ajili ya kuyachakata kiwandani hapo.