Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA), imetangaza kuanza kuwashughulikia wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya mifugo wasiofuata sheria na kanuni zinazoongoza utekelezaji wa shughuli hizo.
Dkt.Bitanyi amewataka wazalishaji wote wa vyakula vya mifugo hapa nchini kuzalisha vyakula vyenye uwiano sahihi wa viinilishe vinavyohitajika kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa na mamlaka ya kuthibitisha ubora wa vyakula hivyo (TBS) na viwango vya kimataifa kwa wale watakaohitaji kusafirisha nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt.Stella Bitanyi, alipokuwa akitoa taarifa fupi ya yaliyobainika wakati wa operesheni maalum iliyoendeshwa na timu ya wataalam, kutoka Ofisini kwake kwa kushirikiana na wakaguzi wa vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutokana na ukaguzi katika viwanda vinavyozalisha na maduka yanayouza vyakula hivyo katika mikoa ya Dar-es-salaam na Pwani.
Dkt.Bitanyi amewataka wazalishaji kuhakikisha wanapima malighafi zote wanazotumia kutengeneza vyakula vya mifugo huku pia akiwaelekeza kusajili Taasisi na mahali wanapozalishia vyakula hivyo.
Akitoa malekezo upande kwa wa wauzaji wa vyakula hivyo, Dkt. Bitanyi amewataka kuhakikisha wananunua vyakula vyao kutoka kwa wazalishaji waliothibitishwa kwenye viwango vya ubora kwa kila kundi la chakula wanalotaka kununua kwa wazalishaji hao.
Akizungumza mara baada ya kutembelewa na timu ya wataalam hao mmoja wa wazalishaji wa vyakula vya Mifugo kutoka mkoani Pwani Bw. Samson Maro ameipongeza Serikali kwa kufanya zoezi hilo mara kwa mara ambapo ameahidi kuyafanyia kazi yale aliyoshauriwa na wataalam hao.
Naye mmoja wa wauzaji wa chanjo na Vyakula vya kuku na bata kutoka mkoani humo Bi. Domitila Melisa amewaeleza wataalam hao namna anavyowasaidia wafugaji waliopo kwenye eneo lake kwa kuwapa elimu na ushauri kuhusu aina ya chakula wanachopaswa kupewa ndege hao kulingana na umri walionao.
Akizungumzia hali yake ya ufugaji kabla ya kupewa elimu inayohusu vyakula vya mifugo, Mfugaji wa kuku kutoka Kibaha mkoani Pwani Bi. Mwajuma Mwami amesema kuwa alikuwa akinunua vifaranga na chakula cha kuku wake kwa kubahatisha jambo lililokuwa linasababisha vifo vya mara kwa mara vya vifaranga hao ambapo ameiomba Serikali kufanya zoezi la ukaguzi na uhakiki wa viwanda na maduka ya vyakula vya mifugo kuwa endelevu.
Uzalishaji wa vyakula vya mifugo nchini unasimamiwa na sheria ya Nyanda za malisho na chakula cha mifugo ya mwaka 2010 pamoja na kanuni zake zilizoandaliwa mwaka 2013, ambapo kwa pamoja vinawataka wazalishaji na wauzaji wa vyakula hivyo kuhakikisha wanyama wanapata vyakula bora ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao yao.