Back to top

WAZIRI ASHATU:TUMIENI VEMA FURSA ZA SOKO LA AFCFTA

30 January 2024
Share

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji na Mwenyekiti wa Mkutano wa 13 wa Mawaziri wa Biashara,  wa Eneo Huru la Biashara Afika (AfCFTA) amezisisitiza nchi Wanachama wa Mkataba huo, kutumia vema fursa zilizopo ili kukuza biashara.
 
Dkt. Kijaji ameyasema hayo, alipokuwa akifungua Mkutano wa 13 wa Mawaziri wa Biashara AfCFTA, unaofanyika Durban, Afrika Kusini, Mkutano huo ambao utafanyika kwa siku mbili  kuanzia tarehe 30 hadi 31 Januari 2024.

Aidha amezitaka nchi hizo kuendelea kushirikiana katika kukamilisha Itifaki ya Uwekezaji, Itifaki ya Biashara ya Kidigitali, pamoja na majadiliano kwenye Vigezo vya Uasili wa Bidhaa na kukamilisha masuala muhimu yanayohusu mifumo ya utatuzi wa migogoro katika ufanyaji biashara kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara.

Akifafanua zaidi,  Dkt Kijaji amesema ushirikiano wa nchi  hizo  kupitia AfCFTA , utachangia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya usafirishaji wa barabara, reli na usafiri wa anga, usalama, ukosefu wa nishati ya kutosha, uzalishaji mdogo na mawasiliano.
 
Mkutano huo wa 13 wa Mawaziri ulitanguliwa na mikutano kadhaa katika ngazi ya Wataalam ikiwemo Mkutano wa 16 wa Kamati ya Makatibu Wakuu pamoja na mkutano wa 10 wa masuala ya Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara  iliyofanyika Januari 23 hadi 29, 2024.