
Waziri wa Ujenzi Mh. Innocent Bashungwa amewatoa hofu Wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam, wanaotumia usafiri wa vivuko eneo la Kigamboni -Magogoni juu ya taharuki kuhusu huduma inayotolewa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) nakueleza kuwa imetengenezwa na watu wenye maslahi binafsi.
"Ningependa kuwatoa wasiwasi wananchi wa Dar es Salaam pamoja na Kigamboni, taharuki ambayo imetengenezwa, hakukuwa na sababu ya kutengeneza hii taharuki, yapo maslahi binafsi nyuma ya utengenezaji wa hii taharuki, lakini ningependa kuwaomba wananchi wa Kigamboni pamoja na Dar es Salaam, waendelee kuwa watulivu waendelee kuwa na subira.” Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Ujenzi akitoa ufafanuzi kuhusu taharuki inayoendelea kutokea kuhusu utoaji huduma kivuko Magogoni Kigamboni .
Ameeleza kuwa sasa vivuko vingi vinaendelea na matengenezo, lakini pia Mkandarasi Songoro Marine anaendelea na ujenzi wa vivuko vipya katika karakana yake mkoani Mwanza kwa ajili yakupelekwa kwenye maeneo mbalimbali kutoa huduma kwa wananchi.
Aidha, Bashungwa amesema kuwa tayari ameikutanisha TEMESA na Kampuni ya AZAM Marine na kujadili namna bora yakushirikiana kwa pamoja kuboresha utoaji huduma ya usafiri wa vivuko katika eneo la Magogoni - Kigamboni.
