
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula ameipongeza jamii ya wawindaji ya Wahadzabe iliyopo wilaya ya Mkalama mkoani Singida kwa utayari iliyouonesha wa kutambua na kukubali kupimiwa maeneo yao na kupatiwa hatimiliki za kimila.
Jumla ya hatimiliki za kimila 100 zikiwemo 26 zinazomilikiwa kwa pamoja kati ya mke na mume zimetolewa kwa jamii ya wawindaji ya Wahadzabe ikiwa ni hatua kubwa kutokana na jamii hiyo kujishughulisha zaidi na uwindaji, utafutaji matunda, urinaji asali na uchimbaji mizizi.
Dk. Mabula amesema hatua hiyo inaonesha nia na dhamira njema waliyonayo ya kutaka kuyalinda maeneo yao wenyewe na kwa kushirikiana na serikali.
‘’Hakika hizi ni salamu na ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa jamii ya wawindaji inaungana naye na mkoa tayari kwenda naye sambamba katika kuletea watu wote maendeleo’’ amesema Dk. Mabula.
Akizungumza na wananchi wa jamii ya wawindaji ya Wahadzabe katika kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza wilaya ya Mkalama amesema, jamii hiyo ni miongoni mwa jamii ndogo nchini ambayo iko katika hali ya kupoteza ardhi wanayoimiliki kutokana na jamii nyingine kuingia na kufanya shughuli zisizoendana na tamaduni za jamii hiyo jambo alilolieleza linahatarisha ustawi na maisha na desturi za Wahadzabe.
