Back to top

Waziri Dkt. Kalemani atoa mwezi mmoja kwa mameneja Tanesco.

21 April 2018
Share

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametoa mwezi mmoja kwa mameneja wote wa mikoa wa shirika la umeme nchini Tanesco kuwaunganishia umeme wananchi wote ambao tayari washalipia huduma hiyo na meneja atakayeshindwa kutekeleza agizo hilo ajiuzulu kazi mara moja.

Akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme vijijini, REA , awamu ya tatu katika maeneo mbalimbali wilayani Kyela, Waziri wa nishati Mhe.Dkt. Medard Matogolo Kalemani amesema ipo kero ya wananchi wanaolipia huduma ya kuunganishiwa umeme kukaa muda mrefu bila kupewa huduma hiyo, kero ambayo amesema hataki kuisikia tena, hivyo akaagiza kila mwananchi anayelipia huduma hiyo aunganishiwe umeme ndani ya siku saba, huku akitoa mwezi mmoja kwa mameneja wa mikoa wa Tanesco nchini kuhakikisha wanawaunganishia umeme wateja wote waliokwishalipia huduma hiyo.

Waziri wa Nishati - Mhe.Dkt. Medard Matogolo Kalemani 

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Cloudia Kitta akamweleza waziri Dkt.Kalemani kuwa kuna kata tatu ndani ya  wilayani yake ambazo hazijafikiwa kabisa na miradi ya kupatiwa umeme, na kumuomba kata hizo ziingizwe kwenye mkakati wa kupewa umeme kupitia mpango wa rea awamu ya tatu.

Mkuu wa Wilaya ya Kyela - Cloudia Kitta.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kyela, Hunter Mwakifuna ameishukuru wizara ya Nishati kuwa kuwaelekeza wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini kuwashirikisha viongozi wa maeneo husika, hatua ambayo imepunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela - Hunter Mwakifuna.