Back to top

WAZIRI DKT.MABULA ATAKA MIPANGO YA KUSIMAMIA ARDHI.

02 July 2022
Share

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula ametaka kutengenezwa kwa mipango bora ya kusimamia ardhi kwa lengo la ardhi kubaki katika ubora wake wa matumizi yaliyokusudiwa kwa wanyama na binadamu.

Amesema kutengenezwa kwa mpango wa matumizi bora ya kusimamia ardhi kutaisaidia jamii kwa ujumla pamoja na kutunzwa kwa ardhi kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Dkt.Mabula amesema hayo katika Kituo cha Urithi wa Utamaduni mkoani Arusha wakati aliposhiriki Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mfuko wa Wanyamapori wa Afrika (Africa Wildlife Foundation). 

Maadhimisho hayo yaliambatana na Maonesho ya Tuzo za Picha zilizopewa jina la Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa (Benjamin Mkapa African Wildlife Awards).

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wizara yake inayo furaha kufanya kazi na jamii ikiwemo Mfumo wa Wanyamapori wa Afrika katika juhudi za kusimamia rasilimali kwa manufaa ya binadamu na wanyamapori.

Ametaka washiriki wa maadhimisho hayo kujiuliza namna watakavyoweza kushiriki katika kuhakikisha mazingira yanakuwa salama, ardhi inatunzwa sambamba na kupangiwa matumizi mazuri ya kuishi binadamu na wanyama bila kuleta taharuki.