Waziri Jafo atangaza uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga kidato Tano.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe Suleiman Jafo ametangaza uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2018 huku akiwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya Tanzania Bara kuhakikisha wanatimiza azma ya kila tarafa kuwa na shule ya kidato cha tano

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Waziri Mhe Jafo amesema ni azma ya serikali ya awamu ya tano kuhakikisha kila tarafa inakuwa na shule ya kidato cha tano ili kuwawezesha wanafunzi wote wanaofaulu mitihani ya kidato cha nne kupata nafasi ya kuendelea na masomo.

Waziri Jafo amesema Jumla ya wanafunzi 70,904 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano ,vyuo vya ufundi na vyuo vya elimu ambapo wasichana ni 31,884 na wavulana ni 39,020.

Aidha Waziri Jafo amesema endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti kwa zaidi ya siku 14 nafasi yake itachukuliwa na mwanafunzi mwingine aliyekosa nafasi ambapo amewataka wazazi na wanafunzi kuzingatia taratibu za kuripoti kujiunga na kidato cha tano.

Katika kipindi cha mwaka 2017 jumla ya watahiniwa laki tatu kumi na saba elfu mia saba sabini na saba walifanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne kati yao elfu tisini na tano mia tatu thelathini na saba walifaulu kwa kupata alama za daraja la kwanza hadi la tatu.