Back to top

Waziri Lugola kuyafuta makampuni ya ulinzi yanayoajiri Vikongwe.

19 July 2019
Share

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema Serikali itayafuta makampuni ya ulinzi binafsi nchini ambayo yanaajiri askari vikongwe  na wasiokuwa na mafunzo mgambo wala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Lugola amesema wizara yake haiwezi kucheza na masuala ya ulinzi na usalama wa nchi kwa kuyaacha makampuni hayo yakiendelea kuajiri vikongwe ambao hawawezi kushika silaha za moto na pia mara kwa mara wanasinzia kiasi kwamba muda wowote wanaweza wakanyang’anywa silaha na majambazi ambao wanazitafuta  kwa ajili ya kufanyia uhalifu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa wananchi wa kata ya Nansimo, jimbo la Mwibara, wilaya ya Bunda Mkoani Mara,amesema kutokana na upungufu wa askari, serikali iliruhusu kuwepo na makampuni binafsi ya ulinzi kwa ajili ya kusaidia masuala ya ulinzi na usalama nchini, lakini baadhi ya makampuni hayo yanavunja sheria kwa kuajiri walinzi wasiokuwa na mafunzo yoyote.

Lugola amesema, kutokana na changamoto hiyo, Serikali inakaribia kukamilisha kuwepo na sheria ya makampuni hayo ya ulinzi, ambayo itasimamia vizuri makampuni yote nchini, na sheria hiyo itaenda kudhibiti pia masuala ya ajira askari hao.