Back to top

WAZIRI MABULA ATAKA WAMILIKI WA ARDHI KUMILIKI MAENEO KWA HATI

11 August 2023
Share

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula, amewataka wamiliki wa ardhi nchini kuhakikisha wanamilikishwa maeneo yao kwa kupatiwa hatimiliki za ardhi ili kuwa na salama ya miliki zao.

Dkt.Mabula alisema hayo wilayani Makete mkoani Njombe, wakati wa kukabidhi hatimiliki za ardhi kwa wananchi wa wilaya hiyo akiwa katika ziara yake ya siku tatu katika mkoa huo.

Amesema wananchi wa Makete waliojitokeza kuchukua hati mara baada ya kukamilisha taratibu za umilikishwaji wamechukua uamuzi sahihi unaoenda kuwahakikishia usalama wa milki zao.

Amebainisha kuwa, mmiliki wa ardhi mwenye hati mbali na kuwa na salama ya miliki yake lakini hati hiyo inampa fursa nyingi ikiwemo kuhukua mikopo benki pamoja na kuitumia kama dhamana.

Hata hivyo, Dkt Mabula alishangazwa na idadi ndogo ya wananchi wanaojitokeza kuchukua hati ambapo alisema kati ya wamiliki 88 wa wilaya ya Makete waliothibitisha kwenda kuchukua hati katika tukio la kukabidhi hati ni wamiliki 25 tu waliojitokeza na kukabidhiwa hati zao.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kuwawezesha wananchi kupitia ardhi zao na uwezeshwaji huo ni kuwa na umiliki halali  wa ardhi unaowapa salama ya maeneo yao sambamba na kuwawezesha kutumia hati katika kujiwezesha kiuchumi.

Amesema, wamiliki wa ardhi wanaojua alama za mipaka katika maeneo wanayomiliki ni tofauti na wale wanaomiliki maeneo wakiwa na hati zao na kueleza kuwa wanaopatiwa hati wana shughuli nyingi za kimaendeleo wanazoweza kuzifanya kupitia hati.

Kwa upande wao Wananchi wa Makete waliokabidhiwa hati milki za ardhi waliishukuru Wizara ya ardhi kupitia waziri mwenye dhamana kwa kuwapatia hati milki za ardhi amabpo walisema huko nyuma ilikuwa vigumu kuzipata.

Faidon Kyando mkazi wa Makete aliyekabidhiwa jumla ya hati sita na Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula alisema hakuamini alipopigiwa simu akitakiwa kwenda kuchukua hati za maeneo yake hasa akiwa na kumbukumbu za huko nyuma kusikia kwamba kuna mtu alichukua hati kwa kiasi cha milioni mbili.

Jumla ya wamiliki 25 kati ya 88 wa ardhi katika wilaya ya makete mkoani Njombe walikabidhiwa hati milki za ardhi na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula katika tukio lililohudhuriwa pia na Mkuu wa mkoa wa Njombe Athony Mtaka pamoja na mbunge wa jimbo la Makete Festo Sanga.