Back to top

WAZIRI MABULA AWATAKA MAAFISA SEKTA YA ARDHI KUJITATHMINI, IRINGA

01 December 2022
Share

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula amesikitishwa na watendaji wa sekta ya ardhi katika Halmashauri za Manispaa na Wilaya ya Iringa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, na kusababisha Halamshauri hizo kushindwa kukusanya maduhuli ya serikali yatokanayo na kodi ya pango la ardhi.

Amewataka maafisa ardhi wateule katika Halmashauri hizo, kujitathmini kutokana na kushindwa kwao, kwenda na kasi ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha wananchi wanamilikishwa na kupatiwa hatimiliki za ardhi.

Akiwa katika ziara ya siku moja mkoani Iringa, kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi, Dkt.Mabula amebaini uzembe wa baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi, wakiwemo maafisa ardhi wateule kwa kushindwa kusimamia utoaji hati za ardhi na uingizaji milki za ardhi kwenye Mfumo wa Utunzaji Kumbukumbu za ardhi kwa njia ya Kielektroniki.

Waziri Dkt.Mabula amewataka maafisa hao wa sekta ya ardhi katika Halmashauri hizo mbili za mkoa wa Iringa, kuhakikisha mwezi Disemba mwaka 2022 wawe wamewasilisha taarifa zao za makusanyo ya kodi ya pango la ardhi pamoja na hatua walizochukua kwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi.

Ameongeza kwa mtendaji wa sekta ya ardhi hajui idadi ya viwanja vilivyopo kwenye mfumo wa utunzaji kumbukumbu za ardhi, anawezaje kudai madeni? na kubainisha kuwa wamiliki wa ardhi wanapotambulika kwenye mfumo  inakuwa ni rahisi kwa watendaji kudai madeni.

Pia amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri katika mkoa wa Iringa, kutimiza wajibu wao wa kuzisimamia sekta za ardhi kwenye halmashauri zao kwa kuwa idara za ardhi ni za kwao na si za wizara na kubainisha kuwa watendaji wa sekta ya ardhi ni chachu ya kutoa elimu katika masuala ya ardhi.

Aidha ameongeza kuwa, kwenye ziara yake hiyo amekutana na watumishi wa sekta ya ardhi kutoka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Iringa pamoja na wale wa halmashauri ya Manispaa na  Wilaya ya Iringa lengo likiwa kuboresha utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Mkoa wa Iringa unazo jumla ya halmashauri tano ambazo ni Manispaa ya Iringa, Mafinga Mji, Irinda DC, Kilolo DC na Mufindi DC.