Back to top

Waziri Mkuu aagiza gari la wagonjwa lipelekwe Ifakara.

17 September 2019
Share

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupeleka gari la kubebea wangonjwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni kilichopo Halmashauri ya Mji wa Ifakara ili kuwapunguzia wananchi gharama ya kukodi gari kwa sh. 800,000 pale wagonjwa wao wanapopata rufaa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Septemba 17, 2019) wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Ifakara katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa kituo cha mabasi cha mji huo, amesema iwapo fedha za makusanyo ya mapato ya ndani  katika halmashauri husika zingekuwa zinatumika vizuri kusingekuwa na changamoto  kama hizo.

Pia, Waziri Mkuu ameielekeza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ihakikishe katika mgawo wa ujenzi wa hospitali za wilaya, Halmashauri ya Mji wa Ifakara ipewe kipaumbele kwa sababu eneo hilo ni kubwa na lina watu wengi lakini hakuna hospitali ya wilaya hivyo kusababisha msongamano mkubwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni.

Awali, Mganga Mfawidhi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Dkt. Happyness Ndosi alisema kituo cha Afya cha Kibaoni kinapokea na kuwahudumia wagonjwa wa  nje 225 hadi 250 kwa siku na wagonjwa wanaolazwa ni kati ya 50 hadi 80 kwa siku. Wakinamama wanaojifungulia kituoni hapo ni 400 kwa mwezi.

Akizungumzia kuhusu changamoto zinazikabili kituo hicho amesema kina upungufu wa watumishi 92, kwani kina jumla ya watumishi 83 huku mahitaji yakiwa ni watumishi 175,  ukosefu wa gari la wagonjwa na pia hakina gari lolote la kutolea huduma zikiwemo za chanjo, na usambazaji, uchakavu kwa baadhi ya majengo kama la wagonjwa wa n je.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali haitokuwa na msamaha  na watendaji wa halmashauri watakaobainika kutafuna fedha za makusanyo ya mapato ya ndani pamoja na fedha zinazotolewa kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye maeneo yao.