Back to top

Waziri Mkuu aagiza kumsimamisha kazi Ofisa wa Forodha mpaka wa Mulongo

10 October 2018
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amechukizwa na biashara za magendo zinazoendelea katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, hivyo amewataka viongozi wa wilaya hiyo wajipime wenyewe.

Aidha, amemuagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA mkoa wa Kagera Bwana ADAM NTOGHA kumsimamisha kazi Ofisa wa Forodha katika mpaka wa Mulongo Bwana PETER MTEI kwa tuhuma za kujihusisha na biashara za magendo.

Ametoa maagizo hayo alipozungumza na viongozi wa mkoa wa Kagera katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani humo kilichofanyika mjini Bukoba.

Waziri Mkuu amesema katika mwalo wa Mulongo ulio kwenye mpaka wa Tanzania, Rwanda na Uganda biashara za magendo zinafanyika na hakuna kiongozi anayechukua hatua.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA asiwahamishe watumishi wabovu kutoka kituo kimoja cha forodha na kuwapeleka kingine kwa kuwa huko wanakowapeleka wanakwenda kuendeleza biashara za magendo na kuikosesha serikali mapato.

Amemuagiza Meneja wa TRA wa mkoa wa Kagera Bwana ADAM NTOGHA afanye ukaguzi kwenye vituo vyote vya forodha katika mkoa huo pamoja na kuongeza idadi ya watumishi na kudhibiti vitendo vya rushwa.