Back to top

Waziri Mkuu akanusha taarifa ya shule, vyuo kufunguliwa leo.

25 March 2020
Share

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao kwamba vyuo na shule vitafunguliwa kesho siyo za kweli.
 
Taarifa hiyo ambayo haioneshi chanzo chake kama ni ya kwenye televisheni au kwenye blog, imeunganisha kauli ya TAMISEMI na kuweka picha ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikionesha kwamba vyuo na shule vitafunguliwa Jumatano bila kuonesha ni Jumatano ipi.


 
Jumanne iliyopita (Machi 17, 2020), Waziri Mkuu alitangaza kuwa shule zote za awali, msingi na sekondari zitafungwa kwa siku 30 ili kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19).
 
Na siku iliyofuata (Jumatano, Machi 18, 2020), Waziri Mkuu alitangaza kwamba vyuo vyote vya elimu ya kati na vya elimu ya juu vitafungwa kwa muda wa siku 30 ili kuondoa msongamano katika maeneo hayo na kuweza kujikinga na virusi vya corona.
 
Alisema mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima imesitishwa kuanzia siku hiyo ikiwemo shughuli za michezo, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali na shughuli nyingine za kijamii.