Back to top

Waziri Mkuu azindua zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura.

18 July 2019
Share

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua rasmi zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwahimiza vijana waliotimiza miaka 18 wajitokeze kwa wingi kujiandikisha.
 
 Waziri Mkuu ametoa rai hiyo wakati akizindua zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika kwenye uwanja wa Mandela, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
 
Amesema zoezi hilo ambalo limeanza leo, linafanyika kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Amesema litafanyika nchi nzima na linatarajiwa kukamilika Machi, 2020.
 
 Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziasa asasi za kiraia ambazo zimepewa vibali vya kutoa elimu ya mpigakura, zijiepushe na ushabiki wa kisiasa na badala yake zizingatie mwongozo wa elimu ya mpigakura uliotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Amesema ana imani kuwa wananchi wakipata elimu kuhusu uboreshaji kama inavyoendelea kutolewa, basi watahamasika kutumia haki yao ya kikatiba ya kujiandikisha katika daftari hilo na hatimaye kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.