Back to top

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ampongeza Rais Dkt.Magufuli.

12 June 2020
Share

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya India, Mhe. Narendra Modi amempigia simu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambapo viongozi hao wamezungumzia masuala yahusuyo uhusiano na ushirikiano mzuri, wa kirafiki na kihistoria uliopo kati ya Tanzania na India.

Katika mazungumzo hayo Mhe. Modi amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake wa Awamu ya Tano na amemtakia heri yeye na Watanzania wote katika juhudi kubwa za kuijenga nchi zinazoendelea na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Pamoja na kumhakikishia kuwa India itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania katika nyanja mbalimbali hasa kiuchumi, Mhe. Modi amempa mrejesho wa yaliyojiri katika mkutano wa nchi 20 tajiri duniani (G20) uliofanyika hivi karibuni (India ikiwa ni mojawapo) ambapo nchi hizo zimekubaliana kuwa taasisi za fedha za kimataifa zitoe msamaha wa madeni kwa nchi masikini na zinazoendelea, zilizopata madhara kutokana ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).