Back to top

WAZIRI NDAKI ATAKA MAZAO YA UVUVI KUNUNULIWA MASOKONI

03 February 2022
Share

Waziri wa Mifugo na uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewaagiza Watendaji wa wizara hiyo kwa kushirikiana na Watendaji wa Halmashauri kote nchini kuhakikisha wafanyabiashara wanaotoka nje ya nchi wananunua mazao ya uvuvi katika masoko yaliyopangwa na serikali na sio kwenye mialo  kama baadhi yao wanavyofanya sasa ili kuepuka kupoteza mapato ya serikali yatokanayo na mazao hayo. 

Waziri Ndaki ametoa agizo hilo wakati alipofanya kikao kilichohusisha watendaji wa wizara ya mifugo na uvuvi (sekta ya uvuvi), wafanyabiashara na wadau wa sekta hiyo kutoka halmashauri ya jiji la Mwanza.

Ameto magizo hayo baada ya wafanyabiashara  wanaofanya shughuli zao katika soko la Kimataifa la Kirumba kumweleza  kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara kutoka mataifa ya jirani ambao wananunua mazao ya uvuvi katika mialo badala ya kwenda sokoni na kusababisha serikali kukosa mapato.

“Kama kuna wafanyabiashara kutoka nje ya nchi wanakwenda kununua mazao ya uvuvi huko visiwani, hao wanatenda makosa, wanapaswa wakamatwe na wafunguliwe mashitaka, naomba mamlaka husika kuanza kufuatilia malalamiko hayo ili kukomesha upotevu wa mapato,” amesema Mhe. Ndaki

Ametumia nafasi hiyo pia kusema kama kuna baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali wanashirikiana na wafanyabiashara hao nao watafuatiliwa na kupelekwa kwa mamlaka zao husika ili wachukuliwe hatua.