Back to top

WAZIRI NDAKI AWASHAURI WAFUGAJI KUFUGA KIBIASHARA.

05 January 2022
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewashauri Wafugaji nchini kufuga kibiashara na kuachana na ufugaji wa kuchunga ambao tija yake imekuwa ndogo kwao wenyewe na hata kwa Taifa pia, waziri Ndaki ametoa rai hiyo alipotembelea shamba la kisasa la mifugo la Shaffer lililopo Mkoani Iringa.

Akiwa katika shamba hilo akikagua shughuli mbalimbali zinazoendelea kwenye eneo hilo amesema kuwa wanawashauri wafugaji kuanza kufuga kisasa na kuachana na ufugaji wa kiasili ambao sasa umeanza kupitwa na wakati.

"Tumekuwa hatuoni faida kwa mifugo yetu kwa sababu ya kung'a ng'ania ufugaji wa kiasili, wafugaji tuanze  kufuga kibiashara ili tuongeze tija ya mifugo yetu", amesema Mhe.Ndaki.

Ameongeza kuwa ili waanze kuona tija ya ufugaji wao ni lazima wabadilike na waache ufugaji wa kuzunguka kutafuta maeneo ya malisho na badala yake wawe na maeneo yao ya kufugia ambayo yatakuwa rahisi kufikiwa na Wataalamu kwa ajili ya kuwapatia huduma zinazohitajika kwa mifugo yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bw.Bashiru Muhoja amesema kuwa Muwekezaji wa Shamba hilo la Mifugo la Shaffer anauhitaji mkubwa wa chakula cha mifugo yake kama vile soya na mahindi. 

"Mhe. Waziri huyu mfugaji anauhitaji mkubwa wa soya, mahindi na alfaalfa ambapo kwa sasa vyote anavitoa nchini Zambia, hii ni fursa kwa wananchi wetu na tumeshaanza kuchukua jitihada na tunaorodha ya wakulima ambao wapo tayari kulima mazao hayo kwa ajili ya kumuuzia mfugaji huyu", Amesema Muhoja

Kwa upande wake, Msimamizi wa Shamba la Shaffer, Bw.Mahboob Malick ameeleza kuwa wanaishukuru serikali kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa inaowapatia na kwamba wako tayari kuendelea kushirikiana nayo kwa lengo la kuboresha ufugaji hapa nchini.

"Mhe. sisi tuko tayari kupokea vijana ambao wanataka kujifunza ufugaji waje hapa tutawafundisha namna bora ya ufugaji wa kisasa ili wakipata ujuzi huu waende kuwafundisha na wenzao na hatimaye kuboresha ufugaji wetu", Amesema Malick.